SSPRA

JOIN SSPRA TO ACQUIRE PUBLIC RELATIONS SKILLS

Thursday, March 7, 2013

Padri Kitima na maajabu ya SAUT


PADRI Charles Kitima alipoteuliwa kuwa makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Mt Agustino (SAUT), Mwanza mwaka 2004, hakuna aliyekuwa na wazo kwamba miaka kumi ya uongozi wake angeweza kufanya maajabu ya kukifanya chuo hicho kuwa hivi kilivyo.


Akishika nafasi ya mtangulizi wake, Padri Kamugisha, aliamini kuwa amepewa kazi kubwa na nzito katika taifa. Nayo ni kupigana na moja ya maadui wakubwa ‘ujinga’. Hivyo, aliazimia kutumia nguvu, akili, maarifa na wakati mwingine kuteseka kwa ajili ya maendeleo ya chuo hicho.

Kasi yake ndiyo inayowashangaza wengi ndani ya kanisa na nchi kwa ujumla, ambapo atakapokabidhi madaraka kwa mwenzake Julai mwaka huu, Padri Kitima anaicha SAUT ikiwa ndicho chuo kikuu pekee nchini chenye idadi kubwa ya wanafunzi, matawi mengi na maendeleo ya kuridhisha.

Chuo Kikuu cha SAUT kilianzishwa rasmi mwaka 1998 ikiwa ni mafanikio ya kilichokuwa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Nyegezi (Nyegezi Social Training Institute) kilichoanzishwa tangu mwaka 1960 na Wamisionari wa Kanisa Katoliki ambao kwa sasa wanajulikana kama Wamisionari wa Afrika chini ya Askofu Mkuu Joseph Blomjous wa Jimbo Kuu la Mwanza.

Mwanzoni mwa miaka ya 1960 kilikuwa ni kipindi ambacho nchi nyingi za Afrika zilipata uhuru ikiwemo Tanzania. Kutokana na wimbi la mabadiliko katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara, Wamisionari wa Afrika walitambua kuwa ujuzi katika suala la habari na mawasiliano, maendeleo ya jamii, uhasibu, usimamizi na utawala vilihitajika kuendelezwa ili kuelimisha wafanyakazi ambao wangechukua uongozi katika nchi za Afrika Mashariki na Kati ambazo zilikuwa zimepata uhuru.

Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Nyegezi (NSTI) ililenga kutoa mafunzo ya kitaaluma na kitaalamu, lakini pia kutoa maadili ya elimu ya uraia na kijamii kwa wazawa bila kujali rangi au imani katika nyanja hizo kuu za elimu.

Askofu Joseph Blomjous alipostaafu mnamo mwaka 1964, alikabidhi taasisi kwa mrithi wake, Askofu Renatus Butibubage ambaye aliongoza taasisi hii hadi mwaka 1975 alipoikakabidhi rasmi kwa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC).

Hadi kufikia mwaka 1998 zaidi ya watu 2,400 walikuwa wamepata mafunzo katika taasisi hii kwa ajili ya kutoa huduma katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Tangu mwaka 1992 kulikuwa na hoja mbalimbali ndani ya Serikali ya Tanzania, ikiwamo suala la utoaji wa huduma za kijamii kuwa huria. Hivyo mwaka 1996 ukawa mwaka kikanisa ulioazimia kupanua huduma ya elimu ya chuo kikuu.
Hivyo, Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Nyegezi, ikapandishwa hadhi na kuwa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (St. Augustine University of Tanzania-SAUT), chini ya TEC kikikubali mamlaka ya sheria ya Canon (Canon Law) na katiba ya Apostoliki (Apostolic-Constitution) “Ex-Corde Ecclesiac” kwa ajili ya vyuo vikuu Katoliki.

Chuo cha Mtakatifu Augustino kimeanzishwa kwa mujibu wa sheria za nchi na kinafanya kazi chini ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa mujibu wa masharti ya vyuo vikuu sheria namba 7 ya mwaka 2005.

Haikushangaza kuona kwamba ndani ya muda mfupi wa uongozi wa Kitima, mamia ya wanafunzi kutoka nchi nyingi za Afrika Mashariki kama vile Kenya na Uganda pamoja na za bara la Ulaya, Amerika, na Australia walivutiwa sana kuja kusoma katika chuo hiki.

Dira na maono
Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania waliamua kupanua huduma ya utoaji wa elimu ya juu katika maendeleo ya mtu na heshima kwa utu wa binadamu.

Lengo la kuanzishwa kwake
Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino kililenga kuwa kituo cha ubora wa elimu, utafiti na utumishi wa umma; kukuza harakati na ulinzi wa kweli, uwazi na uaminifu, pamoja na umahiri na kujituma katika utoaji huduma; kujenga na kuendeleza dhamira ya kutunza mali binafsi na mali ya umma; kuhamasisha maendeleo ya jumla kwa kutoa elimu bora juu ya uwezo wa uchambuzi na dhamira ya kutoa huduma kwa ukarimu na heshima kwa binadamu.

Mafanikio yake tangu 1998
SAUT kilipoanza mwaka 1998 kimefanikiwa chini ya uongozi wa Padri Kitima, kimeongeza matawi mengine mapya 13 katika kanda mbalimbali hapa nchini, na kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka wanafunzi 204 hadi 13,121 kwa mwaka wa masomo 2012/2013.

Chuo kimeongeza vitivo vingine vinne (4) kutoka kitivo kimoja cha Sayansi ya Jamii na Mawasiliano ambacho kilikuwa na shahada moja ya Mawasiliano ya Umma. Kimefanikiwa kujenga madarasa mapya, na majengo ya utawala ambayo yamesaidia sana kuongeza ufanisi katika utoaji wa elimu bora.
Chuo kimefanikiwa kutoa elimu kwa wazawa juu ya kuwekeza katika ujenzi wa nyumba za kuishi wanafunzi (hostel) ambazo zimewawezesha kujipatia kipato na pia kuwapa elimu ya biashara ndogondogo.

Kinachofundishwa SAUT
Tangu chuo kuanzishwa mnamo mwaka 1998 kumekuwa na ongezeko la programu mbalimbali ambazo zimekuwa zikiongezwa kwa awamu tofauti.
Hii ni kutokana na tafiti makini na za kina zinazofanywa na wahadhiri wa chuo ndani na nje ya nchi, ambazo zimekisaidia kutambua umuhimu na uhitaji wa programu mbalimbali katika maendeleo ya jamii, Afrika na duniani kwa ujumla. Programu hizi zimegawanyika katika vitivo vifuatavyo:

Kitivo cha biashara na utawala:
Shahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Biashara, Sayansi katika Ugavi, Utalii na Usimamizi. Nyingine ni Stashahada ya Juu katika Ununuzi na Usimamizi katika Ugavi na Uhasibu. Pia kinatoa elimu ya cheti katika Utawala wa Afya na Ugavi.

Kitivo cha Sayansi ya Jamii na Mawasiliano:
Hiki kinatoa elimu ya Shahada ya Uzamivu katika Mawasiliano, Uchumi, Mawasiliano ya Umma na Maendeleo ya Jamii. Kinatoa pia Shahada ya Mawasiliano ya Umma na Masoko, Uchumi, na Maendeleo ya Jamii. Kadhalika kinatoa elimu ya cheti katika Uandishi wa Habari.


Kitivo cha elimu:
Kitivo hiki kinatoa elimu kiwango cha Shahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Mipango ya Elimu, Usimamizi wa Maendeleo ya Elimu ya juu na katika Isimu.
Pia kinatoa Shahada ya Sanaa na Elimu, Shahada ya Falsafa na Elimu na Shahada ya Mafunzo ya Dini na Elimu.

Kitivo cha Sheria:
Kwa sasa kitivo hiki kinatoa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sheria, na Shahada ya Uzamili katika Sheria. Kadhalika kinatoa Shahada ya Sheria.

Kitivo cha Uhandisi:
Hiki kinatoa elimu ngazi ya Shahada ya Sayansi katika Uhandisi Ujenzi, Shahada ya Sayansi katika Uhandisi Umeme pamoja na cheti katika Teknolojia ya Habari.

Changamoto
Wahenga wanasema “kwenye msafara wa mamba na kenge hawakosekani”, ndivyo ilivyo katika Chuo cha Mtakatifu Augustino, kwani pamoja na mafanikio yaliyopatikana tangu kilipoanzishwa yapata miaka 14 sasa, kumekuwa na changamoto mbalimbali. Hizi ni pamoja na ucheleweshwaji wa malipo ya ada kwa wanafunzi wanaolipiwa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.
Changamoto hii imekuwa ikijitokeza kila mara na kwa muda mrefu hali ambayo imesababisha chuo kuchelewa kutekeleza baadhi ya shughuli za maendeleo ya elimu.
Nyingine ni kuyumba kwa uchumi wa taifa usio imara, na ushawishi wa kisiasa ambao unaweza kuharibu uhuru katika utoaji wa elimu.
Kadhalika kipato cha chini kwa Watanzania walio wengi kunachangia baadhi ya wanafunzi kushindwa kumudu gharama za masomo ya elimu ya juu hivyo kushindwa kuendelea na masomo.

Mafanikio
Dk. Kitima alipoulizwa amewezaje kufanikisha haya ndani ya muda mfupi hadi chuo kikawa na umaarufu kiasi hicho anasema: “Siri ya hatua hii nzuri iliyofikiwa na SAUT inatokana na ubora wa elimu inayotolewa na chuo kwa kuangalia mahitaji muhimu yanayomwezesha mwanafunzi kuwa na uwezo na ufanisi mkubwa wa kujiajiri na kuajiriwa baada ya kuhitimu.
“Katika mtaala wa chuo, wanafunzi wanapata fursa ya kusoma masomo ya ujasiriamali na kujiajiri baada ya kuhitimu masomo yao na hivyo kuondokana na dhana ya kungoja kuajiriwa.”
Anadai kuwa chuo kimeboresha kiwango cha elimu inayotolewa ili kuhakikisha wahitimu wanahimili soko la ushindani Afrika Mashariki na duniani kote, pia kutokana na elimu ya dini na maadili kwa wanafunzi wote.
“Lengo ni kusaidia kujenga maadili mazuri katika jamii kwani sasa upo mmomonyoko mkubwa wa maadili katika ofisi mbalimbali na kukithiri kwa rushwa, ufisadi na mengine mengi sambamba na hayo,” anasema.
Pia wanafunzi wote wanapata fursa ya kusoma masomo mbalimbali yanayomwezesha mwanafunzi kuwa na uwezo na ufanisi mkubwa wa kupambana na kukabiliana na mambo mbalimbali katika utendaji wa kazi, kama vile Kifaransa, Falsafa, Kiingereza, Ujuzi katika mawasiliano, Upembuzi yakinifu (Kufikiri kwa kina), Takwimu na Uchumi.

Ushirikiano na jamii
Chuo kimefanikiwa kuwawezesha wanajamii wa Kata ya Mkolani, hususan Kijiji cha Sweya ambapo kimewafadhili kupitia kikundi chao cha Muungano katika shughuli zao za ujasiriamali. Kila mwaka chuo hutoa kiasi cha shilingi milioni 20 kwa kikundi hicho.
Kimefanikiwa kutoa misaada ya vitabu mbalimbali kwa baadhi ya shule za msingi zilizo karibu na mazingira ya chuo kupitia shughuli mbalimbali za kitaaluma zinazofanywa na wanafuzi kwa jamii.
Chuo kimefanikiwa kutoa mafunzo ya maadili kwa wanafunzi wote, ambayo ni msaada mkubwa kwao katika utendaji wa kazi hasa katika kipindi hiki cha sayansi na teknolojia.
Kimefanikiwa na kinajivunia kuanzisha mashindano ya mpira wa miguu, mpira wa pete, kikapu, meza na riadha yajulikanayo kama “PRO-LIFE” (Promote Life) kuanzia mwezi Agosti hadi Februari kila mwaka.
Pia mashindano ya FAWASCO kuanzia mwezi Machi hadi Juni. Mashindano haya yanajumuisha jumla ya shilingi milioni 40 pamoja na fursa ya kutembelea nchi mbalimbali za Afrika Mashariki kwa mshindi wa kwanza na wa pili.
Chuo pia kimefanikiwa kuanzisha kituo cha kuzalisha na kuwawezesha wajasiriamali (Business Incubation Centre) ambapo wanafunzi wanaohitimu wanapata fursa ya kuandika mawazo yao ya biashara na baada ya mawazo yao kukubalika wanapatiwa mafunzo maalumu juu ya mawazo yao ya biashara na kisha wanapatiwa mtaji kati ya shilingi milioni 25 hadi 30 kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za ujasiriamali.

Wito kwa wadau
“Tunaiomba serikali kuandaa mazingira bora hasa kwa wahitimu kwa kuwapa mikopo stahiki kupitia asasi za serikali kama benki ili waweze kutumia ujuzi walionao hasa kiujasiriamali na kuleta maendeleo kwa mtu binafsi na taifa kwa ujumla.
“Tunaishauri serikali na sekta binafsi kuwatumia wasomi mbalimbali katika mipango ya maendeleo ya nchi ili wananchi waweze kufaidi matunda ya wasomi kwa maendeleo ya taifa,” anasema Dk. Kitima na kuongeza:
“Serikali pia inapaswa kuboresha elimu ya msingi na sekondari ambayo haswa ndio kitovu cha ubora wa elimu, ili kusaidia taasisi za elimu ya juu kupata wanafunzi wa kutosha na wenye sifa sitahiki.”
Anasema serikali inapaswa kuviangalia vyuo binafsi na kuviwezesha angalau kwa kuvipatia ruzuku kwa ajili ya miradi yake ya maendeleo, kwamba hii itasaidia kuongeza kasi ya maendeleo na kukuza ubora wa elimu ya juu hapa nchini.


“Serikali inapaswa kutimiza wajibu wake wa kutoa mikopo kwa wakati ili kuepuka migomo na maandamano yasiyo na tija kwa jamii,” anasema na kuwataka wananchi wawe mstari wa mbele kuwekeza katika elimu ya juu kwa kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo na si kuwaachia watu wa nje au nchi jirani kufanya hivyo.
Kwa upande wa wananchi, anashauri wakazi wa Kanda ya Ziwa hususani Mkoa wa Mwanza, Wilaya ya Nyamagana mahali ambapo chuo kipo, kushirikiana nacho katika kuwalea na kuwahudumia wanafunzi kwa malazi na ulinzi ili kudumisha amani na mshikamano.

“Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi nchini kuendeleza ushirikiano katika suala la ulinzi na usalama katika eneo la chuo na sehemu za makazi ya wanafunzi wetu ili waweze kusoma kwa amani na utulivu.
“Tunatoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji mbalimbali kukiunga mkono chuo chetu katika kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile ujenzi wa madarasa, vifaa vya kufundishia kama vile kompyuta na vitabu mbalimbali.

“Tunatoa wito kwa wanafunzi wote wa SAUT wawe na moyo wa upendo na kujali mali za chuo, pia washiriki vyema katika shughuli za kitaaluma na michezo ili kutunza heshima ya chuo ndani na nje ya nchi,” anasema.
Anatoa wito kwa wahadhiri wote wa SAUT kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kufikia dira ya chuo ambayo ni kuendelea kuwa kituo cha ubora na mafanikio katika elimu ya juu na huduma kwa jamii.

http:Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment